Mpango wa Mungu wa Wokovu

Wokovu ni jambo lingine ambalo halieleweki vizuri kwa baadhi ya watu katika imani ya Kikristo, Kuna wakristo wanaokataa na wengine kudhihaki kuwa hakuna wokovu duniani na kwamba wanaoamini katika wokovu wamechanganyikiwa. Aidha utata mwingine katika suala la kuokoka ni pale ambapo baadhi ya watu wanaoamini kuwa kuna wokovu wanapodai kwamba mtu hawezi kuokoka akiwa hai bali kuokoka ni hadi mtu akishafariki dunia!

Hayo ni mawazo potofu na inasikitisha inapoonekana kuwa hata baadhi ya viongozi wa makanisa hawalielewi vizuri suala hili ambalo ni muhimu katika imani ya kikristo kwani ndiyo sababu hasa iliyomleta Bwana Yesu duniani, kuja kuwaokoa watu. Mtume Paulo anasema kwamba; “Ni neno la kuaminiwa, tena  lastahili kukubalika kabisa; ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni ili awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi”. 1 Timotheo 1:15. Hivyo Wokovu kwa wanadamu ni mpango wa Mwenyezi Mungu mwenyewe kwa kadri alivyoamua kwamba iwe hivyo. Kutoeleweka vizuri kwa suala hili matokeo yake ni watu kuyumba au kuyumbishwa katika imani, na hata baadhi ya wanaodhani wanaelewa maana yake wakijikuta wakiwa nje ya ukweli.
Aidha kwa yeyote anayejiita mkristo lakini anakataa kwamba hakuna wokovu basi hana haki ya kujiita mkristo. Kwani Ukristo siyo tu kuwa na majina yanayoitwa ya ‘kikristo’; bali Ukristo ni imani; ni kufuata mfano wa Yesu mwenyewe. Mtume Petro anawaelezea wakristo kwa kusema kuwa; “Kwa sababu ndiyo mliyoitiwa Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake”. 1 Petro 2: 21.
Wokovu unapatikana kwa Yesu Kristo pekee, unapo okoka na kuishi maisha ya utauwa, Roho wa Kristo anakaa ndani yako. “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awayeyote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake”.Warumi 8:9. Hivyo unapokuwa hujaokoka unakuwa umepoteza sifa ya kuwa mkristo kulingana na maandiko hayo hapo juu; ambayo yanasema kwamba mtu yeyote asipokuwa na roho wa Kristo huyo si wake.
Mlinzi wa gereza walimofungwa Paulo na Sila kule Filipi baada ya kushuhudia nguvu za Mungu aliwauliza Paulo na Sila afanyeje ili aweze kuokoka; “Kisha akawaleta nje akasema ‘Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?’ wakamwambia ‘mwamini Bwana Yesu nawe utaokoka pamoja na nyumba yako...”. Matendo ya Mitume 16:30-31. Mlinzi yule wa geraza alifahamu kuwa Paulo na Sila walikuwa ni watumishi wa Mungu kwani kosa lililowafanya wafungwe lilikuwa ni kuwahubiria watu njia ya wokovu.
Wokovu upo na unapatikana kwa wanadamu waliohai kupitia kwa Bwana Yesu Kristo na si vinginevyo. Biblia takatifu inafundisha kuhusu wokovu. Yaani maana nzima (main theme) ya Neno la Mungu ni Wokovu. Injili inahubiriwa duniani kote ili watu wamjue Mungu kisha waokoke. Bwana Yesu mwenyewe amelielezea suala hili katika mfano alioutoa kuhusu maisha ya tajiri na maskini Lazaro ambapo baada ya wote kufariki; Lazaro alikwenda peponi na yule tajiri alikwenda motoni. Kwakuwa wakiwa huko walikuwa wakionana; yule tajiri kutokana na mateso  aliyokuwa akiyapata aliomba Lazaro atumwe ulimwenguni kuwaeleza ndugu zake tajiri huyo  hali ya mateso anayopata mtu asiyeokoka anapofariki dunia na hivyo kuwataka nduguze hao watubu dhambi zao wakiwa hukohuko duniani kwani hakuna nafasi ya kutubu baada ya kifo. Soma Luka 16: 19-31.
Wanao puuzia suala la wokovu wasijione kuwa wako sahihi na salama, Neno la Mungu  linasema kwamba;  “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu”.
1 Wakorintho 1:18.
Hata kuja kwake Bwana Yesu kwa njia ya kuzaliwa kulivyotabiriwa ilielezwa wazi kuwa huyo Yesu angekuja kuwaokoa watu wake na dhambi zao. Ina maana watu walio hai siyo waliokufa.  ----“Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao”.
Mathayo 1: 21
Kupitia Nabii Yoeli Mungu alisema kuwa watakuwepo watu watakao okoka, maana yake ni watu walio hai siyo wafu. “Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayelitaja jina la Bwana ataponywa, kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako  watu watakao okoka, kama Bwana alivyosema na katika mabaki, hao awaitao Bwana”. Yoeli 2:32
Kupitia Nabii Isaya Mungu anasema; “Jikusanyeni mje, na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka! Hawana maarifa wale wauchukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga, wamwombao mungu asiyeweza kuokoa”. Isaya 45:20.
Kwa kuwa kila atakaye liitia jina la Bwana ataokoka;
Warumi 10:13. , wenye uwezo wa kuita ni watu walio hai siyo wafu na je Jina hilo ni lipi? Maandiko yananasema kwamba jina hilo ni Yesu. “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana Jina jingine chini ya Mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” Matendo 4: 12.
Yesu aliema kwamba mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia Yesu awezaje mtu kuzaliwa akiwa mzee? Aweza mtu kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yohana 3:3-4. Yesu alimaanisha kuokoka.
Waliookoka wanalo jukumu muhimu la kuwatangazia wengine habari njema ya wokovu kwani  Mungu huwatumia watu hao, hivyo si vyema kujifungia ndani na wokovu wako kwani utakuwa hujatimiza wajibu wako, ni sawa na kuifukia ardhini talanta uliyopewa badala ta kuifanyia biashara ikazaa na kuongezeka; Mungu anasema;“...Wakati unakuja nitakapokusanya watu wa mataifa yote na lugha zote ; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu. Nami nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa”. Isaya 66:18-19.
Kunapo kuwepo watu waliookoka hiyo ni ishara ya uwepo wa Mungu mahali hapo.
Wokovu ni Nini?
kuokoka si kujiunga na kanisa la kiroho wala  kuokoka si kuambiwa na mchungaji fulani maneno ya kutamka na ukishamaliza kutamka maneno hayo mchungaji huyo anakuthibitishia kuwa tayari umeokoka. Eti kwa sababu maandiko yanasema kuwa ukimkiri Yesu kwa kinywa chako kuwa ni Bwana utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kuambiwa maneno ya kutamka na mtu mwingine siyo kuokoka. Hayo ni mapokeo, huko ni kupotosha maandiko kwenye lengo la labda kutaka kuongeza idadi ya waumini katika kanisa husika bila kujali kama kuna dhamira ya dhati ya mtu huyo ya kutaka kuokoka  inayotokana na kuelewa Neno la Mungu.
Aidha kwakuwa matukio mengi ya namna hiyo yanatokea katika mikusanyiko ya watu makanisani au katika mikutano ya hadhara; watu ambao inakuwa mara yao ya kwanza kufika mahali hapo labda kwalengo tu la kutaka kujua kinachofanyika, hujikuta wakiulizwa kama wako tayari kuokoka! Wengi wao labda kwakuhofia kueleweka vibaya na waumini wengine au ndugu waliokwenda nao mahali hapo, ndipo hulazimika kukubali pasipo kuwa na dhamira ya dhati. Matokea yake, watu wa aina hiyo wengi wao hawafuatilii tena mafundisho. Watu wanatakiwa wafundishwe neno la Mungu ili waijue kweli kisha waamue wenyewe wakikiri kwa vinywa vyao kwa kutamka maneno yao wenyewe siyo kwa kuambiwa maneno ya kutamka kwani suala hilo ni kwaajili ya maisha yao ya baadaye. Mtu yeyote makini hakubali kulazimishwa kupokea kitu asichokijua faida na hasara zake, hali kadhalika kumpokea Yesu wasiye mjua ni sawa na kufanya mzaha katika imani. Wachungaji na viongozi wa makanisa wasikwepe kutimiza wajibu wao wa msingi wa kuhubiri injili kwa kila kiumbe ili watu waokolewe. Wasikimbilie kukamatia watu wasioelewa kwani hawatadumu nao.

Kuokoka ni kumkiri Yesu kuwa ndiye Mungu pekee aliye hai na hakuna mwingine. Wokovu ni imani, na imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Warumi 10: 17. Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Waebrania 11:1. Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamfuatao. Waebrania 116.
Maandiko yanasema; “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu utaokoka “. Warumi 10: 9 “Jueni ya kwamba Bwana ndiye Mungu, ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake, tu watu wake na kondoo wa malisho yake”.   Zaburi 118:27. HivyoYesu ndiye Bwana  na Bwana ndiye Mungu na jina lake ni Yesu. Yohana 14:7-9;Yohana 17:12
Zakayo mtoza ushuru wa Yeriko alitubu mwenyewe dhambi zake mbele ya Bwana Yesu na Yesu akamthibitishia kuwa wokovu umeingia ndani ya nyumba ile. Yesu ndiye wokovu, alipomwambia Zakayo kuwa wokovu umeingia katika nyumba yake hakumaanisha hali ya kimwili kwa maana ya yeye kuingia katika nyumba ya Zakayo yenye kuta nne bali alikusudia  kwamba Roho wa Mungu ameingia katika mwili wa Zakayo baada ya yeye kutubu dhambi zake na Yesu kumsamehe, ambapo mwenye uwezo wa kusamehe dhambi ni Mungu pekee ambaye Jina lake ni Yesu. Mtume Paulo anatukumbusha kwamba “ Au hamjui kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe”. 1Wakorintho 6: 19.
“---Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba , Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu”. 2 Wakorintho 6: 16-17
Mtume Paulo anasema; “Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sote, naliona  imenilazimu kuwaandikia ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu”. Yuda 1: 3. Pia alisema; “Kwakuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake bali tupate wokovu,kwa Bwana wetu Yesu Kristo”. 1 Wathesalonike 5: 9. Wokovu unapatikana kwa Yesu Pekee kwakuwa ndiye Mungu aliye Roho Takatifu.
“Hili ni zuri , nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu, ambaye hutaka watu wote waokolewe na kupata kujua yaliyo kweli”. 1 Timotheo 2: 3-4. Ukiokoka kikweli kweli utaijua kweli nayo kweli itakuweka huru. Na kweli ni Yesu Kristo na kuijua ni kufunuliwa kutambua kuwa Yeye ndiye Mungu na hakuna mwingine.
Na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema “Njia ni hii, ifuateni”,mgeukapo kwenda mkono wa kulia na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto. Isaya 30:21. Yesu ndiye njia na kweli na uzima.
Hata hivyo wapo wanaosikia na hawaamini kama kuna wokovu, lakini Yesu anasema kwamba; “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile isianguke ; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu , aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga . Mvua ikaja, pepo zikavuma, zikaipioga nyumba ile, ikaanguka, nalo anguko lake likawa kubwa”. Mathayo 7: 24- 27.
Kumbe kusikia Neno la Mungu na kulitii ndicho kipimo cha mtu kuwa na akili kinyume na baadhi ya watu wanaowadhihaki waliookoka kwa kuwaambia wamechanganyikiwa; kwani kwa mujibu wa Bwana Yesu, waliochanganyikiwa ni wale walisikiao neno lake na kulipuuza.
Hata kupitia Nabii Yeremia Mungu anasema; “Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake,wala mwenye nguvu asijisifu kwasababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababau ya utajiri wake. Bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi na kunijua, ya kwamba mimi ni Bwana, nitendaye wema...” Yeremia 9:23-24.
Wokovu umekuwa ukipata upinzani mkubwa katika jamii za watu . Waliookoka wamekuwa wakiitwa majina mbalimbali ya kejeli na dhihaka kwa lengo la kuwakatisha tamaa. Katika jamii ya watanzania kwa mfano; waliookoka wanaitwa ‘Walokole’ jina ambalo limetokana na dharau tu kwa watu hao ingawa hata hivyo limezoeleka na kufikia  hatua ya kukubalika hata na waliookoka wenyewe. Neno ‘walokole’ halipo katika maandiko matakatifu, hata katika kamusi ya kiswahili limeingizwea hivi karibuni likitafsiriwa kuwa ni ‘wakristo walio na imani kali ya dini yao’ tafsiri ambayo pia haiwatendei haki waliookoka kwa maana hiyo siyo tafsiri sahihi. Kuokoka siyo imani kali bali ndiyo imani halisi ya Ukristo. Aidha, neno la Mungu linasema kwamba; “Wokovu u mbali na wasio haki, kwa maana hawajifunzi amri zako”. Zaburi 119:155. Hivyo wanao washambulia walio okoka ni kama hawajui watendalo, ni watu wanaohitaji msaada wa maombi ili nao waijue kweli.
Kwa waliookoka wanapojikuta wakikashifiwa, kutukanwa, kudharauliwa au kunyanyaswa eti tu kwa sababu ya imani yao thabiti, wasikate tamaa wala kusononeka bali waendelee kufurahi na kuamini kwamba wako sahihi kwani ndivyo Bwana Yesu alivyosema kabla kuhusu yatakayowapata watu wake waliookoka, Yesu alisema; “Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, hata na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwaajili ya jina langu. Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu”. Luka 21:16-19
Kati ya maeneo yenye ubishi na upinzani mkubwa kuhusu wokovu makanisa yanaongoza! Lakini hata Bwana Yesu mwenyewe alisema Neno la Mungu litapingwa katika masinagogi (makanisa): “Na watakapo wapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike  kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyo jibu au kusema kwakuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kusema”. Luka 12:11-12
Kufundisha wokovu kinyume na maandiko ya Mungu ndiko kupinga neno la Mungu ambako Bwana Yesu alisema. Wanaofanya hivyo huenda ni kutokana na kutoelewa vema maandiko au wanapotosha watu kwa makusudi ili kujipatia kipato kutokana na sadaka za watu hao jambo ambalo si la kiungwana. Waalimu wa uongo ni wepesi kukosoa mafundisho ya kweli kwa hofu ya kupoteza waumini wao ambao endapo wataijua kweli ni wazi kwamba watawakimbiana na kuwalaani kwa kuwapotezea muda wao bure kwani Yesu alisema ukiijua kweli itakuweka huru. Mungu hafurahishwi na hali kama hiyo kwani anasema; “Kwa maana kuna wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, hasa wale wa tohara, ambao yapasa wazibwe vinywa vyao. Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwaajili ya mapato ya aibu”. Tito 1: 10-11
Kutokana na mafundisho potofu, wokovu umekuwa na picha isiyopendeza miongoni mwa watu mbalimbali katika jamii kiasi cha hata kuwaogopesha baadhi yao wasitamani ahadi hii muhimu ya Mungu kwa wanadamu; yaani kuokoka. Kwa muda mrefu baadhi ya waliookoka wamekuwa wakiishi maisha ya kujidhiki, maisha ya kinyonge, unyenyekevu wa kinafiki na umaskini wa kujitakia kwa kutojishughulisha wakiamini kwamba eti hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyotaka waishi! Huo siyo mpango wa Mungu wala siyo maagizo yake wakati wowote ule.
Lazima ieleweke kwamba kila mwanadamu ana sehemu mbili katika maisha; sehemu ya kwanza ni maisha ya dunia hii ambapo mahitaji yake yote yanapatikana hapa hapa duniani na tutayaacha hapahapa duniani.. Sehemu ya pili ni  baada ya kufariki dunia ambapo wenye dhambi mahali pao walipo andaliwa ni katika lile ziwa la moto na wale watakao ishi maisha ya wokovu (ya utakatifu) hadi mwisho watakwenda mbinguni na kuishi milele pamoja na Bwana Yesu. Mbinguni kuna maisha yake, tofauti kabisa na maisha ya duniani; hivyo ni kituko kwa wanao acha kuishi maisha mazuri ya duniani kutokana na ahadi ya kuishi vizuri mbinguni. Ieleweke ya kuwa vitu vyote vilivyoko duniani na mbinguni vimewekwa na Mungu mwenywe kwa mpango wake.
Kuishi maisha ya kinyonge na kukosa furaha kwa watu walio na uhakika na maisha yao ya baadaye Mbinguni ni jambo lisiloeleweka. Kama unauhakika katika imani yako kwamba maisha ya wokovu yatakufikisha mbinguni kwanini uwe mnyonge? Hata neno la Mungu pia linatutaka tufurahi kwa maana ufalme wa mbinguni ni wetu. Mungu wtu ni Mungu aliye hai, na jaribio la kwanza katika kuthibitisha uwepo wake ni pale utakapo muomba akusaidie kutatua shida zako mbalimbali za kidunia na ombi lako likatekelezwa, bila shaka hapo unakuwa na uhakika zaidi kuwa kweli Mungu wako yupo na anasikia. Hivyo hata ile ahadi ya kuishi maisha ya milele mbinguni ni ya kweli na ataitekeleza. Ingewezekanaje Mungu awabariki wasioamini walio wengi wawe na maisha mazuri sana duniani lakini wewe uliyeokoka uwe umepangiwa kuishi maisha ya kubahatisha. Kitendo cha kuuhusianisha wokovu na maisha ya dhiki ya kidunia kinapotosha ukweli wa kimaandiko na kumdhalilisha Mungu wetu mbele ya wasioamini na kuonekana kama hana uwezo wa kuwasaidia watu wake. Kama Mungu unaye mwamini asipoweza kukusaidia shida zako mbalimbali hapa duniani ukiwa hai unapo muomba, anza kutilia mashaka imani yako kwani utakuwa na uhakika gani kuwa Mungu huyo anasubiri  aje kukusaidia baada ya kufa kwako? “Mungu wetu sisi ni Mungu wa kuokoa...” Zaburi 68:20.
Maisha ya watakatifu walio wengi tunaowasoma katika Biblia Takatifu tunashuhudiwa ya kwamba walikuwa na maisha mazuri  ya neema na wengine walikuwa ni matajiri hasa. Babu yetu Ibrahimu kwa mfano; maandiko yanamwelezea kuwa alikuwa ni tajiri sana kwa kila kitu; “Naye Ibrahimu alikuwa tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha na kwa dhahabu”. Mwanzo 13:2. Hali kadhalika Ayubu, Mfalme Sulemani ndiyo kabisa! Kwani maandiko yanamwelezea kuwa alikuwa ni tajiri kuliko wafalme wote wa dunia na kwamba hakutatokea tajiri yeyote duniani wa kumzidi yeye. Soma  1Mambo ya nyakati 9:22- 28. Yusufu wa Arimathaya mwanafunzi wa Yesu ambaye alimwendea Pilato kuomba mwili wa Yesu akauzike alikuwa ni mtu tajiri  kulingana na maandiko hata aliweza kumudu kununua kitambaa ghali cha kitani kwaajili ya sanda ya kumzikia Bwana  Yesu. Hivyo wanaofikiri kuwa umasikini ni kigezo cha wokovu ni vema wakapitia upya maandiko matakatifu ili wajue kuwa Mungu haangalii sura ya nje ya mtu kama tufanyavyo sisi wanadamu bali Bwana huutazama moyo wa mtu. 1 Samweli 16: 7.
Aidha Mungu ameahidi baraka kwa wanaoitii sauti yake na kutekeleza maagizo yake yote kwa bidii; vilevile Mungu ameahidi laana kwa wale wasiotaka kuisikia sauti yake na kuacha kutii maagizo na amri zake. Soma Kumbukumbu la torati 28.
Kilicho agizwa kwa matajiri katika maandiko matakatifu ni kwamba; “Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala waiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha. Watende mema wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo; huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli”. 1 Timotheo 6: 17-19.
Kwa wanaoacha kufanya kazi ili kujipatia mahitaji yao kwa kisingizio cha kuokoka; ikiwa ni kwa kuamua wenyewe, wajue kuwa huo ni uvivu, na ikiwa hatua hiyo inatokana na mafundisho ya baadhi ya viongozi wa dini basi wajue kuwa wamepotoshwa. Uvivu na kutopenda kujishughulisha ni machukizo mbele za Mungu. Mtume Paulo anaikemea hali hiyo katika barua yake kwa Wathesalonike kwa kuwaambia ifuatavyo;
“Kwakuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili: Kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi asile chakula. Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine, basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe”. 1 Wathesalonike 3:10-12
Wapo wengine waliothubutu hata kujifungia ndani  wakajilipua kwa moto wakishawishiwa na viongozi wao kuamini kuwa wameokoka na muda wao wa kwenda mbinguni umetimia, wengine  kukusanyika katika maeneo mbalimbali hata misituni wakidai kwamba wana msubiri Bwana Yesu aje awachukue kwenda mbinguni. Matukio ya namna hiyo hayana uhusiano wowote na imani ya Ukristo;  aidha,wanaofanya hivyo wanaidhalilisha imani ya Kikristo kwani BibliaTakatifu  iko wazi kuhusu siku ya mwisho; kwamba ufalme wa mbinguni hauji kwa kuuchunguza chunguza eti uko huku au kule; na pia siku hiyo inaelezwa kuwa itakuja kama vile mwivi ajavyo kuiba, ni ghafla, bila taarifa. Hata hivyo  hakuna sababu ya kuwa na hofu kwa walio okoka hata kama siku hiyo itawakuta wakiwa hai au wakiwa wamekufa kwani neno linasema kwamba;
“kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha  sisi tulio hai, tuliosalia tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa na Bwana milele. Basi farijianeni kwa maneno hayo”.        1 Wathesalonike 4: 16-17
Hata Danieli katika nyakati zake aliwahi kumuuliza Bwana juu ya mwisho wa dunia utakavyokuwa, alisema; “Ee Bwana wangu, mwisho wa mambo haya utakuwaje? Akasema (akajibiwa kwamba) Enenda zako, Danieli, maana maneno haya yamefungwa na kutiwa mhuri, hata wakati wa mwisho, Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe,na kusafika , bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote, bali wao walio na hekima ndio watakao elewa”. Danieli 12:8-10

Hata Mtume Yohana naye anasema kwamba; “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia. Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu, na mwenye uchafu azidi kuwa mchafu, na mwenye haki na azidi kufanya haki, na mtakatifu azidi kutakaswa”. Ufunuo 22:10-11
Endapo hali hiyo inatokana na mafundisho potofu; Bwana Yesu anawaonya viongozi wa aina hiyo wa makanisa  kwamba: “Ole wenu nyie wanasheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, pia na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia”. Luka 11:52

“Basi Roho anena waziwazi  ya kwamba nyakati za mwisho wengine
watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani”. 1 Timotheo 4:1

Ipi ni njia ya Wokovu?

Je una njaa? siyo njaa ya kimwili, lakini kama una njaa ya kitu fulani zaidi katika maisha yako? Je kuna kitu chochote ndani ya nafsi yako ambacho kinakufanya ujione unakikosa? Kama ndivyo hivyo basi Yesu Kristo ni njia, Yesu alisema, "Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kabisa”.
(Yohana 6:35).

Je umechanganyikiwa? Hauwezi kupata ufumbuzi  wa matarajio katika maisha yako? Au ni kama inaonekana kama vile kuna mtu amezima taa katika chumba ulichopo na unashindwa kujua ilipo switch? Kama ndiyo hivyo, Yesu ndiyo njia! Yesu alisema, "Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima" (Yohana 8:12).

Je unajisikia ni kama uliyefungiwa nje? Umejaribu milango yote lakini ukaja kukuta kilichopo nyuma yake ni uwazi na hakuna maana yoyote kwako? Je unatafuta mlango wa kuyafikia maisha yako? Kama ni hivyo, Yesu ni njia! Alisema kuwa; Mimi ndimi mlango, mtu akiingia kwa mimi ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho" (Yohana 10:9).

Je kuna watu wanao kuangusha sikuzote? Je mahusiano yako siku zote ni hafifu na yasiyo na lolote? Je inaonekana kana kwamba kila mtu anataka kutumia nafasi yako kwa faida yake binafsi? Endapo ni hivyo, Yesu ndiyo njia! Alisema, "Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwaajili ya kondoo…Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua ; nao walio wangu wanijua mimi" (Yohana 10:11, 14).

Je, unashindwa kuelewa nini kitatokea baada ya maisha haya ya sasa? Je umechoka kuishi maisha kwaajili ya vitu vinavyooza na kupata kutu? Je wakati mwingine umekuwa ukiwa na mashaka kuhusu maisha kama yana maana yoyote? Je ungependa uendelee kuishi baada ya kufa? Kama ndivyo, Yesu ni njia! Yesu alisema, " Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima.Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi ; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele" (Yohana 11:25-26).

Njia ni nini? Ukweli ni nini? Uzima ni nini? Yesu anajibu maswali hayo kwa kusema kuwa;
"Mimi ndimi njia, na kweli na uzima; mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi" (Yohana 14:6).

Njaa unayojisikia ni njaa ya kiroho, inaweza tu kushibishwa na Bwana Yesu Kristo. Bwana Yesu ndiye pekee anayeweza kuondoa giza katika maisha yako. Yesu ndiye mlango wa maisha yako. Yesu ni rafiki na mchungaji ambaye umekuwa ukimhitaji. Yesu ni Uzima katika maisha ya sasa na yajayo. Yesu ndiyo njia ya wokovu!
Sababu ya wewe kusikia njaa, sababu ya kujiona umepotea gizani, sababu ya kutoona maana ya maisha, ni kwa  sababu umetengana na Mungu. Biblia takatifu inatuambia kwamba wote tumetenda dhambi, na kwamba tumetenganishwa na Mungu. (Mhubiri 7:20; Wrumi 3:23). Pengo unalojisikia katika katika moyo wako ni kukosekana kwa uwepo wa Mungu katika maisha yako. Mungu alituumba ili tuwe na mahusiano naye lakini kutokana na dhambi zetu, tunatengana naye katika mahusiano hayo. Kibaya zaidi ni kwamba dhambi zetu zitasababisha kutengana na Mungu katika maisha ya sasa na maisha yajayo. (Warumi 6:23; Yohana 3:36).

Tatizo hili tunalitatuaje? Yesu ni njia; Yesu alichukua dhambi zetu
(2 Wakorintho 5:21). Yesu alikufa msalabani kwaajili yetu sisi wenye dhambi akachukua adhabu tuliyostahili sisi (Warumi 5:8). Baada ya siku tatu,Yesu alifufuka katika wafu, kuthibitisha ushindi dhidi ya dhambi na mauti  (Warumi 6:4-5). Kwanini Bwana Yesu alifanya hivyo?  Yesu anajibu swali hilo yeye mwenyewe kwamba, "Hakuna upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwaajili ya rafiki zake. " (Yohana 15:13). Yesu alikufa ili tupate kuishi.  Endapo tutaweka imani yetu kwa Bwana Yesu, tukiamini kwamba kifo chake  kimefidia dhambi zetu, dhambi zetu zote zinasamehewa na  kuoshwa; Njaa yetu ya kiroho itakuwa imekwisha. Taa zilizozimwa katika chumba tulichomo zitakuwa zimewashwa tena na kuuona mwanga uliopotea. Tutakuwa na uwezo wa kuyafikia maisha ya neema. Tutakuwa tumemfahamu rafiki yetu wa kweli na mchungaji mwema. Tutakuwa na hakika ya kuendelea kuishi hata baada ya kufa kwetu- maisha ya ufufuo, ya milele mbinguni pamoja na Bwana Yesu.
"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa  Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele" (Yohana 3:16).
Nitakuwaje na uhakika na Wokovu wangu?
Kuokoka ni jambo rahisi, ni suala la uamuzi  lakini kuishi maisha ya wokovu ndiyo kazi ngumu. Maisha ya wokovu ni maisha ya utakatifu hivyo yana majaribu mengi kwani mtu aliyeokoka anakuwa ni mlengwa (target) ya Shetani akikusudia kumwangusha ili asifanikiwe kufika mbinguni na kufurahia maisha ya utakatifu milele. Shetani yeye anayajua maisha hayo kwakuwa aliwahi kuishi huko kabla hajamkosea Mungu na kutimuliwa, hivyo ana wivu na yeyote anaye onyesha nia na juhudi za kutaka kwenda mbinguni. Shetani hana haja ya kuhangaika na watu wasio okoka kwani hao wako upande wake tayari. Tunaona katika Biblia jinsi Shetani alivyohangaika kuitafuta roho ya Ayubu mtu mcha Mungu; ndivyo anavyo hangaika kutafuta roho za watu waliookoka.
Baada ya kuokolewa kwa dhambi, tumeamriwa, “Nenda zako na usitende ghambi tena” (Yohana 8:11).
Tumeamriwa tuishi maisha ya adili, na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa (Tito 2:12) na kuonywa kwamba ishini maisha ya utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao. (Ebr. 12:14)
Ni lazima tumtoleeni Mungu miili yetu kama dhabihu iliyo hai (Rum.12:1), tujitakase na chochote kiwezacho kuchafua miili na roho zetu (2 Kor. 7:1), tujikane urafiki na ulimwengu (Yakobo 4:4).
Kama ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa, itakuaje basi kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi? (1Petro 4:18).
Hakuna awezaye kuishi maisha matakatifu kwa nguvu zake binafsi, bali tu kupitia Roho Mtakatifu.  “Nyinyi mtapokea nguvu na kisha Roho Mtakatifu atawashukieni” (Matendo 1:8).
“Nawaambia vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwaajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu”. Luka 15: 7
Watu wengi sana wamekuwa wakihangaika bila kuwa na uhakika juu ya wokovu wao. Endapo unakabiliana na hali kama hiyo, jiulize maswali yafuatayo ambapo majibu yake yatakusaidia kuwa na uhakika njuu ya uhusiano wako na Mungu.
  1. Hivi ninamwamini Bwana Yesu Kristo kuwa ndiye mbadala kwa dhambi zangu na kumpokea kama mwokozi wangu?
Biblia Takatifu inasema kwamba hiyo ndiyo  njia pekee ya kupata wokovu.
“Bali wote  waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndiyo wale waliaminio jina lake;” (Yohana 1:12).
Hili nalo kwa wengine ambao hawajafunuliwa bado hawaelewi kuwa ni fumbo. Hawajiulizi kwanini maandiko yaseme kuwa ‘wale waliaminio jina lake’. Kuamini jina hilo kunakoelezwea hapa ni kupi? Maana katika hali ya kawaida tu kila anayejiita mkristo anaelewa kwa juu juu kuwa Yesu Kristo ni nani kwake, Hata hivyo hapa anataka afahamike katika uhalisi wake; afahamike vile alivyo; kwamba yeye ndiye Mungu kama alivyojifunua yeye mwenyewe mbele ya mitume wake baada ya kufufuka katika Yohana 14: 7-9.
  1. Je, unaamini hisia kuliko Neno la Mungu katika  kupata uhakika wa wokovu?
Biblia inasema kuwa:
“Amwaminiye Mwana yu na uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hatauona uzima bali ghadhabu ya Mungu inamkalia ,” (Yohana 3:36).
“Amini, amini, nawaambia: Yeye asikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka  yu na uzima wa milele; wala haingii hukumuni , bali  amepita kutoka mautini na kuingia uzimani.”(Yohana 5:24)
  1. Je, unauchukulia wokovu katika mambo unayofanya kwa ajili ya Mungu, Badala ya mambo aliyoyafanya Mungu kwako?

    Biblia inasema kwamba hatuwezi fanya chochote kwaajili ya kupata wokovu. Mungu kutokana na rehema zake amefanya yote yanayohitajika kufanyika.
    “Si kwasababu  ya matendo ya haki  tuliyotenda sisi, bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa mara ya pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu. ”(Tito 3:5).
    “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; amabayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo , mtu awaye yote asije akajisifu. ”        (Waefeso 2:8-9).
    Biblia inasema kwamba tunaweza kuwa na uhakika kwamba tunao uzima wa milele kama tutaamini katika Yesu Kristo kuwa ni mwokozi wetu!
    “Na huu ndiyo ushuhuda: ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika mwanawe. Yeye aliye naye mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini jina la Mwana wa Mungu.” (1 Yohana 5:11-13)
    Siku hiyo ya hukumu Bwana Yesu atasema; “Njooni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni ufalme mliotayarishwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu … kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, “Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa!  Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa ibilisi na malaika zake … basi hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uhai wa milele” (Mat.25:32-34, 41, 46).

Ushuhuda wa maisha ya Kikristo

Imani katika Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu ambaye alikufa kuwa mbadala kwa dhambi zetu  ndiyo kielelezo pekee cha Wokovu. Ufuatao si ushuhuda wa imanin yetu, kwa sababu hatuwezi kuwa na wema wa kutosha kufikia wokovu wa Mungu. Tunaweza tu kutiwa moyo kuwa tuna uzima wa milele kwa sababu Mungu ndivyo anavyosema, kwasababu mabadiliko yametokea katika maisha yetu, kwasababu tunataka kumshiriki Kristo pamoja na wengine, na kwa kuwa tunatamani kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.
  1. Tunatambua kuwa tunao uzima wa milele kwasababu Mungu anasema tunao.
    Neno la Mungu linatuambia ya kwamba tuao uzima wa milele kama tumempokea Kristo kuwa Mwokozi wetu.
“Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini jina la Mwana wa Mungu.” (1 Yohana 5:13)
  1. Tunatambua kuwa tunao uzima wa milele kwa sababu kuna mabadiliko yaliyotokea katika maisha yetu tangu tulipokuwa wakristo.
“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya.” (2 Wakristo 5:17)
Yanaweza kuwa ni mabadiliko madogo. Mwanzoni inawezekana hata yasionekane kwa wengine. Lakini msitari huo unatuambia ya kwamba katika nafasi zetu, tumekuwa mtu mpya tunapompokea Kristo na hivyo mabadiliko katika maisha yetu ni jambo la lazima kutokea.
  1. Tunatambua kuwa tunao uzima wa milele kwa sababu tunataka kumshiriki Kristo na wengine.
“Kwa maana siionei haya Injili; kwasababu ni uweza wa Mungu uletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.” (Warumi 1:16)
  1. Tunatambua  ya kwamba tunao uzima wa milele kwa sababu tunataka kuishi maisha ya ki -Mungu.
“Neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha  kukataa ubaya na tama za kidunia, tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; ” (Tito 2:11-12).
“Maana kwa wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi  Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kasha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa”. 2 Petro 2:20-21.
“Jitunze nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia”. 1 Timotheo 4:16
“Ila mlicho nacho kishikeni sana hata nitakapokuja”.Ufunuo 2:25.
“Imekwisha kuwa Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chamchem ya maji ya uzima,bure.Yeye ashindaye atayarithi haya, mimi nitakuwa Mungu wake naye atakuwa mwanangu”. Ufunuo 21:6.

Comments

Popular posts from this blog

SABABU 100 ZA UKWELI WA SUALA LA SABATO

JINSI YA KUINUA VIZAZI VINGI