UKWELI KUHUSU SABA

Changamoto ya 7: TUNATUNZA JUMAPILI KWA SABABU BAADA YA YESU KUFUFUKA WANAFUNZI WALIABUDU JUMAPILI
a) Tukio la wanafunzi ghorofani siku Yesu alipofufuka(Yohana 20:19-21)
Wale wanaoamini kuwa kuabudu siku ya jumapili ni kuiheshimu siku aliyofufuka Yesu mara nyingi wanazungumzia tukio la wanafunzi waliokuwa ghorofani siku Yesu anafufuka! Kwao mkusanyiko huo ulikuwa ni “kusherekea kwa njia ya ibada ufufuko wa Bwana wao”. Dai hili linashangaza kwani maandiko yanatueleza hivi: Marko 16:9-11,14: “Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwanza alimtoa pepo saba. Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali wanaomboleza na kulia. Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki…..Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine,…. Na hao wakaenda wakawapasha habari wale wengine, wala hao hawakusadiki. Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini kwao, na ugumu wa mioyo yao kwa kuwa hawakusadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu”.Twaweza kuona kwamba waliokuwa hapo ghorofani, hawakuamini kuwa Kristo kafufuka! Itashangaza kama walikuwa wakisherekea ufufuko ambao hawakuamini kama umetokea! Neno la Mungu liko wazi, na linatoa sababu ya mkusanyiko wao “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwa wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu” (Yoh. 20:19).
b) Hotuba ya Mtume Paulo siku ya kwanza ya juma(Matendo 20)
Mdo 20:7, 8: "Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane. Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika"
Fungu hilo hapo juu ni miongoni mwa mafungu yanayotumiwa mara nyingi na rafiki wanaopenda kuhalalisha siku ya jumapili kama siku ya ibada, wakisema kuwa Mkutano wa kiroho uliofanyika siku ya kwanza ya juma ulimaanisha kuhamishwa kwa siku ya ibada toka Sabato hadi jumapili.Hapa hakuna ushahidi wowote kuhusu badiliko la Sabato, wala kuunga mkono wazo la utakatifu wa siku ya Jumapili. Ulikuwa ni mkutano uliofanyika siku ya kwanza ya juma, ambayo sisi tunaiita Jumamosi usiku, lakini pia sio mkutano wa ibada ya kawaida ya Siku ya Sabato. Mambo yafuatayo yanathibitisha ukweli huu:-
i) Ulifanyika usiku. "Palikuwa na taa nyingi” (fungu 8), na Paulo "akafuliza maneno yake hata usiku wa manane” (fungu 7)
ii) Asubuhi yake Mtume Paulo alisafiri. “Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake……. Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimu kusafiri kwa miguu” (mafungu 11, 13).
Usiku pekee wa siku ya kwanza ni ule ambao sisi tunaujua kama Jumamosi usiku[BIBLIA YA KISWAHILI CHA KISASA INAONESHA HILI DHAHIRI]. Siku za Biblia zinaanza na kuisha jua linapozama [machweo] (Mzo1:5; 1:8; Luka 23:54-56; 24:1). Siku ya kwanza ya Biblia huanza jua linapokuchwa [machweo] Jumamosi jioni, na inakwisha jua linapokuchwa Jumapili jioni. Kwa hiyo, "usiku wa manane" ambao Paulo "alifuliza maneno yake" ni lazima ungaliweza tu kuwa, ni ule tunaouita Jumamosi usiku.Hivyo mtume alingoja mpaka Sabato ilipokwisha, ndipo akafanya mkutano wake wa mwisho [wa kuagana](fungu 25) pamoja na ndugu zake kule Troa Jumamosi usiku, naye hatimaye aliendelea na safari yake Jumapili asubuhi. Fungu hili badala ya kuthibitisha utakatifu wa jumapili, linaendelea kuthibitha kuwa jumapili ilikuwa siku ya kawaida ya kufanya kazi ndiyo maana Mtume Paulo anasafiri siku hiyo ya Jumapili Asubuhi.
Jambo jingine ambalo mara nyingi wapendwa wengi wanalitumia kutaka kujiridhisha kuwa mkutano huu ulikuwa ni ibada ya kawaida ni kule kumega mkate kulikotajwa hapa. Lakini Biblia inayo mifano kadhaa ya kuumega mkate ambayo kwa kweli haithibitishi uhalali wowote wa kuifanya siku hiyo iliyotumika kumega mkate iwe siku rasmi ya ibada.
1) Mathayo 26:26: “Nao walipokuwa wakila, Yesu akatwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake akasema, Twaeni mle; huu ndio mwili wangu…. Akakitwaa kikombe akashukuru, akawapa akisema, nyweni nyote katika hiki, kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ajili ya ondoleo la dhambi”
2) Matendo 2:46: “Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe”
Mafungu hayo hapo juu yanatupatia changamoto nyingine pia. Tumeona Yesu akianzisha meza ya Bwana siku ya alhamisi. Kama meza ya Bwana ilimaanisha siku rasmi ya ibada basi alhamisi pia ingekuwa siku rasmi ya ibada. Lakini pia matendo 2:46 inatueleza kuwa “siku zote walimega mkate nyumba kwa nyumba”. Je kila siku ilikuwa siku rasmi ya ibada? Jambo la mwisho pia, tunaona mkutano huu wa Paulo ulifanyika usiku. Siwezi amini kwamba ibada ya kawaida ikasubiri mpaka usiku ndipo ifanyike!
c) Changizo kwa Wakorintho(1Korintho. 16:1-2)
“Kwa habari ya ile changizo kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo. Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapo kuja”
Mjumbe alitumia fungu hili pia kudai utakatifu wa jumapili. Ukweli ni kwamba hakuna rejea yoyote ya kuonesha kuwa Mtume alikuwa akielekeza katika ibada. Michango ilitakiwa “kila mtu aweke akiba kwake” (1Kor.16:2). Suala la msingi ni kwamba kulikuwa na njaa Yerusalemu, hivyo changizo lilikuwa ni kwa ajili ya kuwasaidia ndugu katika Bwana walio Yerusalemu (Rum. 15:26; Mdo 11:26-30).
Matendo 11: 27-30: “Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia. Na walipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uwezo wa roho mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima…….Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadri alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa uyahudi. Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli”.
Paulo alikuwa akiliandikia kanisa la Asia ndogo kuwaomba kutoa msaada kwa Wapendwa waliokuwa na baa la njaa. Fungu hili pia kwa namna moja au nyingine (japo si moja kwa moja) linaweza kuonesha kuwa Sabato waliendelea kuitunza na siku ya kwanza (siku ya kazi) walitakiwa kuanza kwa kuweka akiba nyumbani ili siku Mtume atakapo kuja wasiendelee kuchangishana tena. Fungu hili HALIONESHI UTAKATIFU WOWOTE WA JUMAPILI. Changizo laweza fanyika siku yoyote.Hata hapa kwetu mara nyingi tunakuwa na changizo mbali mbali za ujenzi wa makanisa, kusaidia wahitaji n.k na si lazima zifanyike siku ya ibada C.C. Godfrey Peter,Wilson John, Peter Elisa, Eliapenda Mremi,Onesmo Askaka, Matendo Matende

Comments

Popular posts from this blog

SABABU 100 ZA UKWELI WA SUALA LA SABATO

JINSI YA KUINUA VIZAZI VINGI